Kupanda kilele cha Mlima Kilimanjaro
Nyirenda ni mtu pekee ambaye kamwe hawezi kuachwa katika historia ya aina yoyote juu ya uhuru wa Tanganyika.
Ni yeye aliyepandisha mwenge wa uhuru na bendera katika mlima mrefu kuliko yote Afrika, wa Kilimanjaro Desemba 9, 1961.
Nyirenda alifanya kazi hiyo kwa ujasiri mkubwa, ikikumbukwa kuwa wakati huo, kupanda mlima huo ilikuwa ni jambo kubwa, zito na la hatari kutokana na ukweli kwamba kulikuwa na barafu nyingi na watu wengi waliogopa wakiamini kuwa uwezekano wa kurudi chini ukiwa hai ulikuwa mdogo.
Akielezea tukio hilo, Nyirenda alisema msafara wa kupanda Mlima Kilimanjaro ulikuwa na watu 11, wakiwemo wapiga picha na watangazaji wa redio.
Safari yao ilianza jijini Dar es Salaam kwenda Kilimanjaro ambapo walitumia jumla ya siku 16 kutimiza wajibu huo mzito.
Anasema kabla ya kuanza kupanda, walifanya mazoezi ya kupanda mlima na maandalizi mengine, kwa siku nyingi na siku hiyo walianza kupanda saa 12 jioni na kufanikiwa kufikia juu ya kilele majira ya saa tano usiku.
“Tulianza matayarisho ya kuweka mwenge huku tukiwasiliana na wenzetu wa Dar es Salaam kwa njia ya redio.
“Ilipofika saa sita kamili usiku wa Desemba 9, tuliwasha mwenge tukio ambalo lilikwenda sambamba na kupandishwa kwa bendera ya uhuru wa Tanganyika katika Uwanja wa Taifa wa Uhuru jijini Dar es Salaam,” alisema Nyirenda
Kurejea Dar es Salaam
Baada ya kukamilisha shughuli ya kupanda Mlima Kilimanjaro na kuweka alama hizo muhimu za uhuru, walirudi Dar es Salaam, ambako mji ulikuwa bado ‘ukichemka’ kwa shangwe na nderemo za uhuru kila kona.
“Tulipokelewa kwa furaha kubwa na Rais Nyerere ambaye alikuwa pamoja na mume wa Malikia wa Uingereza (Duke of Edinburgh) ambaye alikuwa amekuja nchini mahsusi kwa ajili ya sherehe za uhuru,” alisema Nyirenda katika mahojiano yaliyofanyika miezi michache kabla ya kifo chake.
Nyirenda alieleza kuwa, Mwalimu Nyerere alikuwa mtu ambaye alijitolea kuwa mtumishi wa dhati, na aliyefanya yote sio kwa ajili yake binafsi bali wananchi wake.
“Alitufundisha kuthamini wengine kwa kuweka neno “sisi” na sio “mimi”, yaani alitufundisha umoja, tuwe pamoja bila kutengana,” alieleza Nyirenda.
Kuugua na kifo chake
Kama kuna jambo lililowasikitisha wengi, ni kutelekezwa kwa muda kwa shujaa huyu baada ya kuanza kuugua ugonjwa wa saratani.
Askari huyu shujaa, alianza kupata msaada wa serikali pale tu vyombo vya habari vilipoanza kuandika na kutangaza habari za kuugua kwake. Ni serikali hiyo hiyo iliyogharamia mazishi yake baada ya kufariki dunia.
Alifikia cheo cha Brigeia Jenerali kabla ya kustaafu rasmi jeshi.
mtanganjia.blogspot.com
Filed Under:
MAKALA
on Sunday, 20 December 2015
Post a Comment