DAR ES SALAAM
WAZIRI MKUU Majaliwa Kassim Majaliwa amewataka wakurugenzi wa vitengo na wakuu wa taasisi katika Ofisi ya Waziri Mkuu (TAMISEMI) wapate nakala ya hansard ya hotuba ya Rais Dkt. John Pombe Magufuli ya kuzindua Bunge la 11, waisome na kufanyia kazi maeneo yote aliyoyaainisha.
“Katibu Mkuu hakikisha umepata hansard ya hotuba ya Mheshimiwa Rais wakati akizindua Bunge na uhakikishe kila mkurugenzi ana nakala na kila mmoja wenu lazima ahakikishe anafanyia maeneo ambayo Mheshimiwa Rais ameyaainisha. Ni lazima tuelewane ni nini tunapaswa tufanye,” alisema.
Ametoa kauli hiyo jana (JANA) mchana (Jumanne, Novemba 24, 2015) wakati akizungumza na wakuu wa taasisi, wakurugenzi na watumishi wa Ofisi ya Waziri Mkuu (TAMISEMI) kwenye mkutano uliofanyika ofisi ndogo ya TAMISEMI, barabara ya Kivukoni, jijini Dar es Salaam.
“Ninatamani kuona mabadiliko ya utendaji kazi Serikalini katika kipindi kifupi. Natamani kila mmoja asiridhike na uzembe unaofanywa huku chini. Ni nyote ni wataalamu, kwa hiyo mnapaswa kudhirisha elimu yenu na ujuzi mlionao,” aliwasisitizia Wakurugenzi hao.
Alisema kila mkurugenzi na mkuu wa taasisi anapaswa kuongeza usimamizi na ufuatiliaji wa kazi kwenye sekta yake kwani hilo litasaidia kukidhi matarajio ya Watanzania ya kuona mabadiliko ya utendaji kazi kwenye Serikali ya Awamu ya Tano.
“Ninyi wakurugenzi siyo desk officers bali ni field officers. Nataka muweke utaratibu wa kwenda vijijini mkasimamie watu wenu, pia mhimize uadilifu, uaminifu na weledi wa kazi,”alisisitiza.
“Mambo ninayotaka mhimize watendaji waliopo chini yenu ni pamoja na haya yafuatayo: muda wa kuripoti kazini uzingatiwe, muda wa kukaa kazini uzingatiwe, utokaji kazini kwenda kwenye chai na chakula cha mchana udhibitiwe, na mipango na malengo ya kazi kwa siku ni lazima yafikiwe,” alisema.
“Tunataka kujua mtumishi amefanya nini tangu alipoingia ofisini. Suala siyo kukaa tu ofisini, kwani kuna mtu anakaa ofisini, hajaenda hata kunywa chai lakini ukiuliza amefanya nini hupati jibu la kueleweka. Sisi kama vongozi wao ni lazima tujue wanafanya kazi gani wanapokuwa maofisini,” alisisitiza.
Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu Majaliwa ameitisha kikao ofisini kwake kesho (LEO )saa 4 asubuhi akitaka kupatiwa taarifa ni kwa nini mradi wa mabasi yaendayo kasi (DART) haujaanza kazi hadi sasa.
“Kesho( LEO) saa 4 asubuhi Katibu Mkuu, Mkurugenzi Mkuu DART na watendaji wako mje ofisini. Nataka kupata maelezo ni kwa nini mabasi hayajaanza kazi hadi leo, je ni lini yataanza kazi, je ni nani anakwamisha. Na hata kama ni sheria, ni kwa nini tusiziharmonise ili kuondoa hivyo vikwazo,?” alihoji Waziri Mkuu.
Post a Comment