Mshambuliaji wa Yanga Amisi Tambwe ameibuka shujaa kwenye mchezo wa leo kati ya Yanga SC dhidi ya Stand United baada ya kutupia kambani bao tatu (hat-trick) na kuifanya Yanga ambao ni mabingwa watetezi wa ligi kuu ya Vodacom tanzania bara washinde mhezo huo kwa bao 4-0 dhidi ya Stand United ‘chama la wana’ kutoka mkoani Shinyanga.
Ndani ya dakika 45 za kwanza, Tambwe alishajihakikishia kuondoka na mpira uwanjani kwani alikuwa ameshamaliza kazi ya kutupia goli zote tatu wavuni.
Tambwe alianza kuzifungua nyavu za Stand United dakika ya 18 akimalizia kazi nzuri iliyofanywa na kiungo mshambuliaji Thabani Kamusoko.
Mrundi huyo hakuishia hapo kwani dakika ya 36 alizama tena nyavuni kupachika bao la pili kwa kichwa na kuifanya Yanga iendelee kuongoza kwa goli 2-0 mbele ya ‘wapiga debe’ wa mjini Shinyanga.
Wakati mchezo unaelekea mapumziko Yanga walifanya shambulizi la kushtukiza ambapo mshambuliaji wa Yanga Donald Ngoma alimiliki mpira kisha kumuwekea mpira Tambwe ambaye moja kwa moja aliachia shuti kali lililomshinda mlinda mlango wa Stand United Frank Muwange na kujaa wavuni dakika ya 45 kipindi cha kwanza.
Thabani Kamusoko aliyefunga bao pekee la Yanga wakati ikiwa mkoani Tanga, alifunga bao la nne kwenye mchezo wa leo dakika ya 62 kipindi cha pili na kuipa timu yake ushindi mnono kwenye mchezo wa leo.
Ushindi huo unawapa Yanga nafasi ya kuendelea kukaa kileleni mwa VPL wakifikisha jumla ya pointi 30 baada ya kushuka dimbani mara 12 msimu huu wakati Stand United wao wamepoteza mchezo wa pili mfululizo baada ya kupigwa kwenye mchezo uliopita wa ‘Shinyanga Derby’ dhidi ya nduguzao Mwadui FC.
FUNGUA HAPA KUSHINDA ZAWADI KEMKEM=>CLICK HERE TO WIN => Click Here=>
Post a Comment