DAR ES SALAAM
RAIS John Magufuli ambaye tangu Novemba 17, mwaka huu alikuwa katika Ikulu ya Chamwino mkoani Dodoma kwa majukumu mbalimbali, amerejea Dar es Salaam jana na wakati wowote inaelezwa kwamba anaweza kutangaza Baraza la Mawaziri linalosubiriwa kwa hamu na Watanzania.
Dk Magufuli alitua Ikulu ya Chamwino, Novemba 17 kwa kutumia usafiri wa barabara akisafiri kwa zaidi ya kilometa 300 kwenda katika Makao Makuu ya Serikali ambako kwanza alikuwa na majukumu mawili makubwa.
Novemba 19, mwaka huu, alimteua Mbunge wa Ruangwa mkoani Lindi, Majaliwa Kassim Majaliwa kuwa Waziri Mkuu na siku iliyofuata alimwapisha katika Ikulu hiyo iliyoko takribani kilometa 40 kutoka Dodoma Mjini.
Aidha, baada ya kumwapisha Majaliwa asubuhi, jioni hiyo ya Novemba 20, Dk Magufuli aliyeingia madarakani Novemba 5, mwaka huu, alilihutubia na kulizindua Bunge la 11 mjini Dodoma katika hotuba iliyosisimua wabunge na Watanzania kwa ujumla kwa kugusa kero na mipango mbalimbali anayokusudia kuifanya.
Dk Magufuli alirejea Dar es Salaam huku tetesi zikiimarika kwamba atatangaza baraza lake la mawaziri siku yoyote kuanzia jana, na aliondoka Dodoma kwa ndege majira ya saa mbili asubuhi.
Kuwapo kwake kwa siku nyingi katika kijiji cha Chamwino akifanya kazi, kulipongezwa na wanakijiji hao. Aidha, wanazuoni na wanasiasa walitafsiri uwepo wake kijijini hapo kuwa ni kujichimbia asibughudhiwe wakati akipanga baraza lake la mawaziri na mfumo wa uendeshaji mpya wa baraza hilo.
Na ishara au dalili kwamba Baraza la Mawaziri limeiva au litatangazwa wakati wowote ni hatua ya Dk Magufuli kutua Dar es Salaam na baadaye mchana kwenda ofisini kwa Majaliwa ambako ni jirani na Ikulu ya Magogoni.
Kwa mujibu wa Katiba ya Tanzania, Rais atateua Baraza la Mawaziri kwa kushauriana na Waziri Mkuu na Makamu wa Rais, hivyo kuna kila dalili wawili hao kama sio wote watatu, wameshafanya kazi hiyo.
Ofisi ya Waziri Mkuu ilithibitisha Dk Magufuli kutinga ofisini kwa Waziri Mkuu, Majaliwa na kufanya mazungumzo ya takribani saa moja.
Post a Comment